Pachanga

Kwa taratibu zetu unapopewa kitu unapaswa kutoa tamko. Na tamko mara nyingi linaambatana na shamrashamra kama vile maji mwenzie matope. Chai mwenzie maziwa. Siagi mkate, na kuendelea. Miriam Odemba aliliuliza hili, tena kwa ghadhabu, kwanini yeye hakutuzwa aliposhinda kuiwakilisha nchi kuchuuza nguo? (Ama kweli, wastara hazumbuki na wa-mbili moja havai!). Mabondia wanatuzwa, na wakimbiaji pia, iweje Bi Mzuri Odemba asituzwe?

Wakati bado tupo katika hili la kutuzana: muda si mrefu uliopita ninakumbuka kusoma kwamba, baada ya kukabidhi nyumba kwa Mwalimu Butiama, wajenzi na wanakijiji walilalamika kwanini hakukuwa na shamrashamra za makabidhiano! Mpunga upikwe, kuku waanguke, Meja Komba aimbe, hayo ndiyo makabidhiano. Au vipi?

Hivi ndivyo mambo yalivyo. Kila ipatikanapo nafasi basi vifijo na vigeregere lazima visikike. Na upatapo nafasi ya kuonyesha anuani yako, hali kadhalika. Utaweka nambari za simu nne, wasifu wako, wewe ni nani katika Jamhuri ya Muungano, na sasa hivi mambo yenyewe anuani za mtandao, hivyo basi unaweka anuani ya Softmail, Warmmail, Rentmail, Chockmail, Dopemail... Hizi ndio shamrashamra zenyewe. Sintopiga vigeregere lakini la kusema ninalo. Kwa kifupi, hili ndio tamko langu:

Pengine wapo mnaodhani nimejitolea kuhukumu yote yanayoendelea hapa. Kama hivi ndiyo, tusameheane. Lengo si kumshushua mtu na wala si kujifaragua. Iweje? Hata mimi ningejenga chuki kama ningedhani unataka kunishushua! Nani, niambieni, anayependa kukoselewa au kusutwa kwa kile alichoandika? Kama yupo, basi tangu leo jina langu Msafiri wa Saba, yule chizi mtaani kwetu aliyekuwa anapenda sana kujadili mambo ya nguoni, hasa baada ya kujisaidia haja kubwa mbele ya duka la Kanji. Hii ni habari nyingine tofauti, hata hivyo, na panapo uhai tutaiongelea.

Hivyo basi, hukumu hakuna. Wote, ninaamini hivi, tupo katika hekaheka ya kutafuta maisha, kila mmoja kwa namna zake, lakini tunaka kujiinua kama wananchi wa nchi moja. Chuki au dharau itoke wapi? Na kama kuna kutofautiana basi ni kutokana na jitahada hii ya kujiinua. Katika historia ya nchi yetu haijawahi kutokea kwa wananchi kutoka nasaba zote wamekaa pamoja kwa mazungumzo ya kila sekunde. Miaka ya karibuni tu, miaka ya themanini hivi, watu walifungwa kwa kuwa na maoni tofauti. Leo tumepata wasaa huu kwanini tusiutumie? (Nilitaka kusema kwanini tusiutumie 'barabara' lakini nitakuwa ninamaanisha nini kwa kusema hivi? Tayari nimeishatoa hukumu kwamba kuna baadhi ya mazungumzo mimi ninadhani 'si-barabara'. Eh, Kiswahili kigumu!).

Tuutumie wakati huu kila mmoja kwa maradhi yake. Anayependa kuongelea soka, na aongelee soka. Ngono (suala la ngono mara nyingi lina utata, lakini ili kuongeza kitu tofauti na yale ambayo wote katika ukumbi tunafahamu kuhusu hili, basi anayejadili inabidi aongeze la ziada: mfano, andika kwa fasaha zaidi ya 'kachojoachupiimeingiakapigamkambi'. Hapa ninamaanisha nini, sijui? Kama ningepata nafasi labda ningejitahidi kuyakinisha. Lakini imani yangu ni kwamba washirika wote wa baraza hili mnaelewa ngono ni kitu gani na hivyo suala liwe ni namna gani unataka kuelezea hiyo ngono ambayo unadhani wengine hawaifahamu.) siasa, uchumi, sheria, biashara, ngano, hali kadhalika. (Bila shaka, haya ni maoni yangu na hapo chini nimeweka saini).

Kila mtu anataka burudani, mabibi na mabwana, na kama burudani zako ni changudoa na Kajumulo, iweje mimi nikwambie, "Hhaahaa, tuzungumzie Marechera? Kesho hatujui hata kama tutaamka, iweje kila mtu aache matashi yake ili tu tuupinge ugandamizaji? Hilo ambalo mimi ninaliona baya linawezekana kabisa kuwa ndilo unalolipenda kuliko yote! Kwangu hili lipo wazi na wala halinikaushi miguu. Furaha, furaha zako. Na zangu, furaha zangu.

Cha msingi kukumbuka: isijekuwa furaha yako ya soka ikawa adha kwa wengine. Au penzi lako kwa Changudoa liondoe usingizi kwa majirani (maana dari hakuna). Labda huu ndio uliokuwa ujumbe wa Ndugu Semboja aliposema, 'Dimbwi huru si uhuru.' Uhuru wa nini cha kuongea ni jukumu la yule anayetuma ujumbe. Binafsi siamini kama kuna uhuru wa kweli katika maoni kwa sababu mbalimbali. Lile ulionalo baya laweza kuwa ndiyo jema kwangu. Hivyo suala, pengine, liwe ni vipi kila mmoja aicheze pachanga kama anavyoijua yeye bila ya kukanyagana miguu.

Kuna baadhi ya mambo ambayo yanatusumbua kama jamaa moja. Masuala ambayo kwa pamoja tumekubaliana (hata kama hatukukubaliana, lakini ili tuishi pamoja nilazima tukubaliane) na kati ya hayo ni masuala ya unyanyasaji kijinsia, rangi, kiuchumi, dini, kabila, umri, sura au hata uzito wa mwili. Imetokea kuna baadhi ya watu katika ukumbi huu wameonyesha dhamira ya kugandamiza wengine kidini mara tu wapatapo nafasi, kwa mfano. Wengine wamejitutumua vidali kunyanyasa wanawake. Sasa, haya kwa kawaida hakuna majadiliano. Nl mambo yanayojieleza wazi kwamba hatuwezi kujadiliana ni vipi nitajisikia kama ukinikashifu kuhusiana na imani yangu.

Vilevile, kuna mwelekeo wa baadhi yetu hapa ambao kutokana na shamrashamra za umri walionao wanataka kufupisha majadiliano. Umri wa mtu, Mabibi na mabwana, ni uzito wa yale unayoweza kuchangia katika mijadala. Vinginevyo hata Msafiri wa Saba (yule chizi mtaani kwetu) siku hizi ana mvi tele (Kama mvi ndiyo tija yenyewe).

Nyakati nyingine wapo wanaozuia mijadala kwa sababu tu, wao ndio wanajua zaidi. Hawa ndio katika wale wanaonza mijadala kwa shutma: 'Askari'. 'Mtu wa Serikali'. Hawa wameishiwa kwani moja ya maana ya kusema 'askari' ni kuonyesha kwamba wao si askari. Jambo ambalo linawezekana kweli au si-kweli. Na usemapo hivi ndio dalili za kutishana kwenyewe. (Umri unakuja tena hapa, wengi wamekulia katika mazingira hayohayo ya miaka ya sabini/themanini wakati wa kudumisha maoni ya kiongozi mmoja. Na ni kweli wapo walioumia kwa kusema yaliyokuwa nyoyoni. Hili linaeleweka au vinginevyo utaanza ubishi wa "Aaa... usituchuuze Bwana wewe hawawezi kukushika!" Nitabaki ninashangashangaa na kung'ang'aa macho, haya yote yameanzaanzaje? La kama kuna mwenye tatizo basi na anyamaze lakini ndo' isiwe tena kutia wengine jangamoyo kwa hofu zako). Huu ni ukumbi wa wanazuoni na kama wapo askari, famil'li laahi, liwalo na liwe lakini hatuwezi kukinga nyoyo zetu kwa hofu ya umbea.

Ningependa kuendelea na changanuo lakini ndo' hivyo tena, muda. Hivyo basi, hakuna chuki mabwana na mabibi pia. Majadiliano na yaendelee na tukosoane kadri tunavyoendelea bila kunyanyasana, umwamba, mbwembwe, uoga au ile kuingiwa na jotomoyo. Kila na mwenye lake na alilete. (Mbali na ukabila-kabila, udini-dini, 'uzee' au uBi-Mkubwa, au kujipachika ushairi usokuwanao, kama mizuka inavyonisuta hapa). 'Wakati ndo' huu', chambilecho na maLatini.

Usiku mwingi.



Hovedside