Bokoboko au Biriani

Nisingependa kuwa mwizi wa fadhila hivyo naomba kuchukua fursa hii kuushukuru uongozi wa 'tanzanet' kwa kuchua uamuzi thabiti na mara moja na kuzima mitambo. Hili ni vyema lieleweke sasa hivi, zaidi ni kutokana na utamaduni tulionao wa kulalamika tu na pale zuri linapofanyika wagumu kutoa shukurani. (Ingawaje haikuwa fadhila kwangu kutoa heshima kwa Mwalimu na kuchukua uamuzi wa 'kuzima' mitambo -sio 'kufunga mitambo'. Unafunga kwa kutumia nguvu).
Mchele una namna nyingi kupikwa (na hata mchele wenyewe una aina nyingi: mamboleo, kitumbili, mchele wa China na kadhalika). Walaji wali hili la matashi mnalielewa. Unaweza kupika biriani, bokoboko, pilau, wali wa maji, wali wa nazi, ubwabwa au uji wa mchele. Inategemea na mpishi, viungo, muda, na hata walaji maana kama walaji wana njaa huwezi kuanza mbindembinde za "...aah ninaweza kupika biriani na pilau kumzidi hata Zamaradi Binti Fikirini!" Suala la msingi inakuwa ni kupika, watu wale. Nakshi za utandu, rangi au upwetepwete wa mchele, vitakuja baadaye.

Katika masuala ya kufurahisha (au kusikitisha, inategemea umeamkaje), ni hili la kululunganya mambo. Una njaa na badala ya kupika unajiuliza biriani au bokoboko? Jaribu kufikiria hili: limetoka pendekezo tutafute njia ya kumpa heshima mmoja wa waasisi wa hadhi yetu kama waTanzania, waAfrika. Nini kinafuatia? Badala ya kwenda moja kwa moja kwenye suala na kusema ama tusizime au tuzime, mtu anaanza mjadala mwingine tofauti. Hapa sina maana kwamba madhali limetoka pendekezo basi tukubaliane kimboliga (aah, kweli lipite). Hasha. Ninachojaribu kusema kwa mtu mwenye fahamu ingekuwa rahisi kujiuliza tu, tuna muda wa kujadiliana? Hatuna. Ninakubaliana na pendekezo? Sikubaliani. Mchezo umeisha. Hivyo unaandika: Siyo wazo zuri, tusizime. Badala yake, mtume si-mama, Bwana wa majeshi na waIsraeli!

Neno dogo litaanza kudoroswadoroswa na mpaka mwisho (au mwanzo kwani hujui tena wapi mkia wapi 'kila-wajinga') habari inakuwa nyingine tofauti kabisa. Matokeo yake hakuna kinachofanyika. Sasa kwa hili na kwa hatua hii, ninaushukuru uongozi ambao, pia hili tukubali, mara nyingi umeshindwa kufikia maamuzi kwa sababu ya hii lulunganya-lulunganya. Nadhani baadhi yetu bado hii hatuifahamu: kama suala ni mjadala (na suala unalielewa) ninaamini kabisa unaweza kujadiliana namna zote. Kulia, kushoto, nyumba, mbele, chini, juu. Au unaweza hata kueleaelea kama mshairi ukawa unanyomoanyomoa tu kama mizuka inavyokutuma. Lakini, cha msingi ni kwamba inafikia wakati ushuke ardhini na kuamua. Bokoboko au pilau?

Au chukulia suala la kuleta ndani ya ukumbi atikali ya Bwana P. J. O'Rourke (jina linanikumbusha viumbe vya Dickens, niwieni radhi kwa kuangua kicheko cha kedi). Fikiria hivi: je, kama atikali isingetumwa ndani ya 'tanzanet' hakungekuwa na sababu ya kukasirishwa? Ghafla tunajadiliana katika ngazi ya chekechea! Bwana wa mabwana, wewe uliye juu mbinguni. Ni kweli atikali haikuwafurahisha wengi wetu lakini hiyo haina maana tungefurahi zaidi kama isingetumwa ali-muradi tusiione tungeridhika! Baya si baya madhali haukuliona! Ili tuelewe kama tumekasirishwa inabidi tuisome atikali na ili tuisome ni lazima atikali itumwe ukumbini. Mbuni toa kichwa shimoni.

Hii ya P. J. O'Rourke ilijengewa hoja kama hivi: "Aaah sasa itakuwaje uitume atikali wakati tupo katika majonzi (timing)? Hili ndio tatizo, tuna huzuni." Lini unadhani hautokuwa na huzuni kama kweli huzuni yako ni ya dhati? Au kwa maneno mengine, je kama ingetumwa wiki mbili baadaye isinge-ghadhibisha? Inawezekana, ninakubaliana nawe, watu tu-tofauti. (Lakini kwa hoja hii ya 'watu tofauti' hata huyo aliyetuma ni mtu, na ana majonzi au furaha zake, hivyo hoja hii inajivunja yenyewe).

(Labda hivi ndivyo inavyopaswa kuwa? Maoni mbalimbali na ndivyo ninavyojifunza, pengine, kuona jambo kwa mitazamo tofauti.) Lakini ili tufike tuendako, kwa maoni yangu, tunahitaji maamuzi na wala sio umahiri wa kuangalia mambo katika madirisha tofauti. Bila shaka, upo wakati wa kuremba na kupambua. Na pia upo wakati wa kuamua kama unataka kula au kutokula kwani suala la wali ni wali gani linakuwa halina tena maana.



Hovedside